NMB, PPRA WAUNGANISHA MIFUMO KIDIGITALI UHAKIKI WA DHAMANA ZA ZABUNI

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, amesema mageuzi ya kidijitali katika sekta ya ununuzi wa umma ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kujenga uchumi jumuishi unaomgusa kila Mtanzania kupitia usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.

Bw. Simba alisema ununuzi wa umma siyo tu mchakato wa manunuzi kati ya mnunuzi na mtoa huduma, bali ni chachu muhimu ya kukuza uchumi wa taifa, hivyo ni lazima uendeshwe kwa uwazi, ufanisi na kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Alieleza kuwa kufuatia maelekezo ya Rais kuhusu mifumo ya serikali kusomana, PPRA imeboresha mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST) na kuanza kuunganisha na mifumo ya taasisi mbalimbali zikiwemo benki, ili kurahisisha michakato ya zabuni.

“Leo tunashuhudia uzinduzi rasmi wa uunganishaji wa mfumo wa NeST na mfumo wa Benki ya NMB, hatua itakayowezesha kuwasilishwa na kuhakikiwa kwa dhamana za zabuni za kibenki kidijitali bila ya usumbufu,” alisema Bw. Simba.

Alifafanua kuwa kupitia mfumo huo, mzabuni ataingiza namba ya dhamana ya benki aliyopewa, na mfumo wa NeST utaivuta moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi bila kuhitaji barua za uthibitisho kama ilivyokuwa awali.

Kwa mujibu wa Bw. Simba, hatua hiyo itaondoa kabisa hatari ya kughushi dhamana za kibenki, kupunguza muda wa uhakiki na kuongeza imani katika mfumo wa ununuzi wa umma.

Aliongeza kuwa kuanzia mwezi Machi 2026, huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki za Benki ya NMB kupitia NeST itaanza kutumika rasmi katika taasisi zote za umma zinazotumia mfumo huo.

Huduma hiyo katika hatua ya awali itahusisha dhamana za zabuni, dhamana za utekelezaji wa mikataba na dhamana za malipo ya awali, ikiwa ni mwanzo wa matumizi mapana ya dhamana za kielektroniki nchini.

Bw. Simba alibainisha kuwa kwa muda mrefu dhamana hizi zilikuwa zikitolewa kwa njia ya karatasi, hali iliyosababisha ucheleweshaji, gharama na hatari ya udanganyifu, hivyo mageuzi haya ni suluhisho la changamoto hizo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, aliwashukuru PPRA kwa kuichagua NMB kuwa benki ya kwanza kuunganisha mfumo wake na NeST katika huduma ya uhakiki wa dhamana za kibenki kidijitali.

Bi. Zaipuna alisema awali mchakato wa uthibitishaji wa dhamana ulikuwa mrefu, ukihusisha kusafirishwa kwa nyaraka na mawasiliano ya barua kati ya taasisi na benki, jambo lililokuwa likichelewesha zabuni na kuongeza gharama kwa wazabuni na taasisi za umma.

Alieleza kuwa kupitia mfumo huo mpya, taasisi za umma sasa zitaweza kuhakiki dhamana moja kwa moja kwenye mfumo wa NeST kwa dakika chache, jambo litakalopunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuimarisha uaminifu katika michakato ya zabuni.

Aidha, alisema ubunifu huo utaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa wakandarasi hawatalazimika tena kusubiri uthibitisho wa muda mrefu kabla ya kuanza kazi.

Bi. Zaipuna aliongeza kuwa hatua hiyo pia itapunguza gharama za uendeshaji kwa benki na wateja wake, kwa kupunguza matumizi ya karatasi, usafirishaji wa nyaraka na muda wa kufuatilia majibu ya uthibitisho.

Alisema NMB imewekeza katika mifumo imara ya teknolojia ya habari ili kuhakikisha usalama wa taarifa na miamala ya kifedha inalindwa kwa viwango vya juu, sambamba na mwelekeo wa serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali.

Bi. Zaipuna alihitimisha kwa kusisitiza kuwa NMB itaendelea kushirikiana na PPRA na wadau wengine kuendeleza mageuzi ya kidijitali, akieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha sekta ya ununuzi wa umma na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania.


    

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

Wasifu wa Kizza Besigye

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

KILA MWANAMKE ANAPASWA KUFAHAMU HII...

IRAN YAMTANGAZA AYATOLLAH MPYA

MBUNGE DKT. MAJULE ATOA MSAADA WA VYAKULA, VYANDARUA 100 SHULE YA VIZIWI DODOMA

MAMBO MADOGO YANAYOVUTIA KWA MPENZI WAKO

DKT. MAJULE AKABIDHIWA CHETI CHA SHUKRANI UWT DODOMA KUFANIKISHA USHINDI WA CCM 2025

MATUKIO RAIS, AMIRI JESHI MKUU DKT. SAMIA AKIZINDUA MAKAO MAKUU YA ULINZI WA TAIFA (MMUT)

WANAOTAZAMWA KUMRITHI AYATOLLAH ALLY KHAMENEI.