USHIRIKIANO WA NMB NA DarTU: HATUA HALISI KUJENGA KIZAZI TAYARI KWA AJIRA

BENKI ya NMB na Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU – zamani TUDARCo), wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) wa Kimakati, wenye lengo la kujenga mfumo rasmi wa uandaaji vijana na kuwajengea maarifa ya kitaaluma, ujuzi wa vitendo na uzoefu wa kukabiliana ushindani wa Soko la Ajira.

Ushirikiano huo wa miaka mitatu, unakwenda kuweka msingi imara wa kuunganisha nguvu kati ya Sekta ya Fedha na Taasisi ya Elimu ya Juu katika kujenga taifa kupitia maendeleo ya rasilimali watu wenye ujuzi, maarifa na uwezo unaohitajika katika uchumi wa kisasa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Jumatano ya Machi 25 jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akonaay, alisema Sekta ya Elimu ni miongoni wa vipaumbele vya benki yake katika mkakati endelevu wa Uwezeshaji kwa Jamii (CSI).

“Elimu ni chachu ya maendeleo na mafanikio ya jamii yoyote. Sisis NMB tunaamini kupitia elimu, tunawaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora na mahiri wa kesho, wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha na kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu. 

“NMB tunayo dhamira ya kusaidia maendeleo ya Sekta ya Rasilimali Watu nchini na hatutosita kuendelea kutumia kila nafasi tutakayopata katika kuunga mkono juhudi za kuboresha maendeleo ya taaluma kupitia fursa za mafunzo kwa vitendo,” alisisitiza Akonaay.

Alifafanua kuwa, kupitia ushirikiano huo benki yake inakusudia kupunguza pengo lililopo kati ya elimu inayotolewa vyuoni na mahitaji halisi ya Soko la Ajira, wakiamini kwamba kwa kufanya hivyo, wanasaidia kujenga kizazi cha wataalamu waliobobea, wabunifu, na wenye uwezo wa kushindana kikamilifu.

“Makubaliano haya na DarTU yanaenda kugusa moja kwa moja katika maeneo yafuatayo: Ukuzaji wa Vipaji na Ujuzi, ambako NMB na DarTU tutashirikana katika kutambua na kuendeleza vipaji kupitia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri.

“Pia, wafanyakazi wa NMB watapata nafasi za kujiunga na Kozi za Muda Mfupi na Programu za Maendeleo ya Kitaalamu za DarTU, hivyo basi kujiongezea ujuzi muhimu na kukuza utamaduni endelevu wa kujifunza,” aliongeza Akonaay mbele ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Burton Mwamila.

Aidha, aliyataja maeneo mengine yatakayoguswa na MoU hiyo kuwa ni pamoja na ushirikiano wa pamoja baina ya NMB na DarTU katika maeneo ya kufanya utafiti pamoja na kushiriki shughuli za jamii, sambamba na ufanikishaji wa maonesho (Career Fairs), na programu za kujenga uwezo na ujuzi kwa wanafunzi na wafanyakazi. 

Aidha, alibainisha ya kwamba ushirikiano huo unaakisi dhamira ya dhati ya taasisi hizo mbili kuwa mstari wa mbele katika uwekezaji wa kimkakati na kuendeleza rasilimali watu, huku ukiwa pia ni uthibitisho wa azma yao ya pamoja ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvu kazi bora.

Akonaay aliongeza ya kwamba wanajivunia ushirikiano huo alioutaja kuwa unaendana vyema na vipaumbele vya kimkakati vya benki yake, pamoja na Maono ya Dira ya Taifa 2050, yanayoangazia umuhimu wa nguvu kazi yenye ujuzi na ubunifu mahali pa kazi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa DarTU, Profesa Mwamila aliishukuru NMB na kwamba wanajivunia ushirikiano huo, ambao licha ya mkataba wao kuwa wa miaka mitatu, utakuwa ukifanyiwa tathmini kila baada ya mwaka mmoja na upo uwezekano mkubwa wa kuurefusha pindi utakapofikia ukomo.

Alisema kupitia makubaliano hayo, DarTU itatoa huduma ya mafunzo na ushauri kwa NMB kama taassisi pamoja na wafanyakazi wake, huku yakiwawezesha wanafunzi wa DarTU kufanya mafunzo kwa vitendo katika benki hiyo, fursa ambayo itawasaidia kulijua soko kabla ya kuhitimu masomo yao.

“Miongoni mwa changamoto zetu zilikuwa ni pamoja na wanafunzi wetu kukosa taasisi za kufanyia mafunzo kwa vitendo ama niite mazoezi, lakini pia kumaliza masomo na kupata shahada zao, wakiwa hawajapata fursa za kujitolea kabla ya kuingia katika Soko la Ajira, changamoto zinazoenda kwisha kwa mkataba huu.

“Lakini pia, sisi hapa tuna shule zinazofundisha nyanja mbalimbali ikiwemo Sheria, Biashara na hata Elimu ya Kidigitali na Huduma za Ushauri, ambako pia tuna Kitengo Maalumu cha Usalama wa Mtandao (cyber security), kinachosaidia sana kutoa elimu ya kuzuia mifumo ya kiusalama ya taasisi kuingiliwa.

“Aidha, sisi kwa sababu ni Chuo cha Elimu ya Juu, tunafuatilia sana maendeleo ya elimu na teknolojia katika maeneo yote na tuko mbele ya muda kuliko taasisi mbalimbali nchini,” alibainish Profesa Mwamila wakati wa hafla hiyo na kuongeza:

“DarTU tunao wajibu mkubwa wa kusaidia kile tulichonacho kuwashirikisha Watanzania zikiwemo taasisi, kwahiyo makubalinao haya yatatuwezesha kuendesha mafunzo ambayo yatawawezesha wafanyakazi wa NMB kwenda na wakati katika maeneo yao ya kazi.”


Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Bw. Emmanuel Akonaay (kushoto) pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini (DarTu), Prof. Burton Mwamila (kulia) wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam. 


Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Bw. Emmanuel Akonaay (wa pili kushoto) pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini (DarTu), Prof. Burton Mwamila (wa tatu kulia) wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni Meneja wa Kanda wa NMB, Bw. Seka Urio na mwanasheria wa NMB, Bw. Fred Abacha (wa kwanza kushoto) na mwanasheria wa DarTu, Bw. Amani Mwakyoma ambapo pamoja na mambo mengine wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini watapata fursa ya kujifunza kwa vitendo NMB kabla ya kuingia kwenye ajira na wafanyakazi wa NMB watapata fursa ya kuongeza elimu ya masuala ya sekya ya kibenki kwenye chuo hicho.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

IRAN YAMTANGAZA AYATOLLAH MPYA

KWA KHERI MAKARANGA UMEUTIMIZA MWENDO...

Wasifu wa Kizza Besigye

KATI YA WATOTO 7 WA HAYATI MAGUFULI ANAYEJULIKANA ZAIDI NI JESCA

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

KIKOSI KILICHOITWA TAIFA STARS HIKI HAPA

KWA NINI MAASKOFU JANA KWENYE IBADA YA KUMUAGA PENGO WALIVAA MAVAZI MEUPE WAKATI NI MSIBA..?

WANAOTAZAMWA KUMRITHI AYATOLLAH ALLY KHAMENEI.

MATUKIO RAIS, AMIRI JESHI MKUU DKT. SAMIA AKIZINDUA MAKAO MAKUU YA ULINZI WA TAIFA (MMUT)