DKT. NEEMA MAJULE AISHAURI RITA KUBORESHA UTOAJI WA VYETI VYA VIFO KWA YATIMA NA WAJANE.



Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Neema Peter Majule, ameishauri Serikali kuboresha utendaji wa Wakala wa usajili, Ufilisi na udhamini (RITA) ili kuondoa ucheleweshaji wa utoaji wa vyeti vya vifo, hali inayowaathiri kwa kiasi kikubwa wananchi hususan yatima na wajane.


Akichangia hoja wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria Aprili 24, 2026, Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Majule amesema RITA ni taasisi nyeti inayogusa moja kwa moja ustawi wa jamii, hivyo kuna haja ya kuongeza ufanisi, kasi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma zake.


Ameeleza kuwa kuchelewa kupatikana kwa vyeti vya vifo kunakwamisha jitihada za yatima wanaotaka kujiendeleza kielimu pamoja na wajane wanaohitaji kukamilisha taratibu za mirathi, akisisitiza kuwa huduma hizo zinapaswa kutolewa kwa wakati ili kulinda haki za makundi hayo.


Katika mchango wake, mbunge huyo pia amepongeza jitihada za Serikali kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign, akisema imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria.


Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusukuma mbele upatikanaji wa haki kwa wananchi, pamoja na Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa juhudi zao katika kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi.


Hata hivyo, amesisitiza haja ya kuboresha zaidi huduma hiyo kwa kuanzisha mfuko maalum utakaowezesha wanufaika wa msaada wa kisheria kupata msaada wa gharama za usafiri na pesa ya kujikimu wanapofuatilia kesi zao.


Aidha, ametoa wito kwa mahakama kuharakisha usikilizwaji wa kesi ili ziweze kumalizika kwa wakati, pamoja na kutumia mbinu za kitaalamu ikiwemo tathmini za kisaikolojia ili kubaini mapema kesi za kubambikiwa na kuhakikisha haki inatendeka bila kuchelewa.




Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

Wasifu wa Kizza Besigye

AINA 10 ZA WANAWAKE AMBAO BIBLIA INAKUONYA UWAEPUKE

MAJANI YA MAPERA NA MATUMIZI YAKE YA KITIBA

RAIS ALİYEISHI KAMA MUNGU WAKATI WATU WAKE WAKIFA NJAA

ZIJUE TIBA ZA MMEA WA MSHONA NGUO.

CHATANDA ASHIRIKI KIKAO CHA BODI HOSPITALI YA RUFAA DODOMA