WAKAZI WA NJOMBE WAFIKIWA NA HUDUMA ZA KIBINGWA MAGONJWA YA MOYO

 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga akizungumza na Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group walioko Mkoani Njombe wanaotoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwenye maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema vilivyopo mkoani humo.

Daktari bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu akimsikiliza mwananchi aliyefika katika banda la JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo katika maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema vilivyopo mjini Njombe

Wananchi wakipata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wakati wa maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema vilivyopo mjini Njombe.

Na JKCI


 

Wakazi wa Mkoa wa Njombe na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao zikiwemo za moyo, huduma inayotolewa na  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group ili kujua hali ya afya zao na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Huduma hizo zinatolewa katika Maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema vilivyopo mjini Njombe.

Akizungumza jana na wananchi waliofika kupata huduma hizo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga alisema kambi hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo kwani ni mara ya kwanza huduma maalumu za moyo kutolewa na wataalamu wa JKCI kupitia maonesho hayo katika mkoa huo.

“Tumefurahi kuona kupitia maonesho haya JKCI mmeleta kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali mkoani Njombe. Ni muhimu wananchi wa mkoa huu  wakatumia fursa hii kujua namba zao za afya na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Mfanga.

Aliongeza kuwa Mkoa wa Njombe utaendelea kushirikiana na JKCI kuhakikisha huduma za kibingwa za moyo zinawafikia wananchi wengi zaidi na kupunguza adha ya kusafiri nje ya mkoa huo kutafuta huduma hizo.

Kwa upande wake Daktari kutoka JKCI Hospitali ya Dar Group  Elius Birago alisema huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ikiwemo moyo ni huduma ambazo zinatolewa na taasisi hiyo katika maonesho hayo na kuwahimiza  wakazi wa Njombe kutumia fursa hiyo kujua namba zao za afya.

Dkt. Birago alisema ni muhimu kwa jamii kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema za kujikinga na magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na kuathili nguvu kazi ya taifa.

“Kutokana na ongezeko la watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo, JKCI tumekuja na kampeni ya Jua Namba Zako za Afya ili kuihamasisha jamii kujua shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uwiano wa urefu na uzito, mapigo ya moyo pamoja na mafuta mwilini”,  alisema Dkt. Birago.

Dkt. Birango alisema jamii ikifahamu viashiria hivyo mapema na kuchukua hatua stahiki itaweza kujikinga na magonjwa hayo na kuishi maisha yenye afya bora.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuweka kambi maalumu za uchunguzi wa afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha jamii kupima afya zao ili  kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

Wasifu wa Kizza Besigye

AINA 10 ZA WANAWAKE AMBAO BIBLIA INAKUONYA UWAEPUKE

MAJANI YA MAPERA NA MATUMIZI YAKE YA KITIBA

RAIS ALİYEISHI KAMA MUNGU WAKATI WATU WAKE WAKIFA NJAA

ZIJUE TIBA ZA MMEA WA MSHONA NGUO.

IJUE HISTORIA YA PACOME ZOUZOUA