MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AZINDUA MATAWI YA NMB

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa wananchi kuepuka wakopeshaji binafsi maarufu kama kausha damu ambao hutoza riba kubwa na kunyanyasa wateja kupitia ukamataji wa mali za wadaiwa. Amebainisha kuwa kufunguliwa kwa matawi mapya ya NMB karibu na wananchi kutatoa fursa ya upatikanaji wa huduma za kifedha kwa ufanisi, usalama, na unafuu.

Dkt. Mpango aliyasema hayo wakati akizindua rasmi Matawi ya Benki ya NMB Chanika na Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa uzinduzi wa matawi hayo utaongeza mchango wa NMB katika maendeleo ya taifa kwa kulipa kodi, kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na kusaidia usalama wa miamala kama malipo ya bili za maji, umeme, ada za shule, na mauzo ya bidhaa.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa NMB kuendelea kuchangia kwenye maendeleo ya kijamii hususan katika sekta za afya na elimu. Alisema kuwa uwajibikaji kwa jamii ndio msingi wa kudumu wa mahusiano bora kati ya benki na wananchi.

“Kupitia kuongeza idadi ya mawakala wenu, mtakuwa mnasaidia kuzalisha ajira kwa vijana ambao ni wadau muhimu wa huduma hizi. Ninaipongeza NMB kwa juhudi hizi na nawasihi msiishie hapa, bali muendelee kuwekeza zaidi katika elimu ya fedha kwa wananchi, hasa wale wa vijijini,” alisema Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa kubuni mikakati bora ya kuongeza uelewa wa masuala ya fedha miongoni mwa wananchi. Aliitaka NMB kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na Umoja wa Mabenki kubuni programu za kuongeza elimu ya kifedha, huku akitoa rai ya kupunguza gharama za huduma za kidijitali ili ziweze kufikiwa na watu wengi zaidi.

Aliongeza kuwa Sekta ya Benki na Fedha imeendelea kukua na kuonesha mafanikio makubwa, ambapo mchango wake kwenye ukuaji wa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.3 mwaka 2019 hadi asilimia 8.6 mwaka 2023. Dkt. Mpango alihimiza NMB kujizatiti kwa mikakati madhubuti ya kuhimili mitikisiko ya kiuchumi, magonjwa, na changamoto nyingine za kimataifa.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alieleza kuwa benki hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha huduma za kibenki zinafika maeneo ya vijijini kwa kuanzisha mawakala na kutumia teknolojia ya kisasa. Alisema lengo ni kuhakikisha kila kijiji nchini Tanzania kinakuwa na mawakala angalau wawili wa NMB ili wananchi wapate huduma karibu yao.

“Tunafahamu changamoto ya idadi ndogo ya watumiaji wa huduma za kibenki vijijini, hivyo kupitia mawakala wetu na uwekezaji kwenye teknolojia, tunahakikisha huduma zinawafikia wananchi popote walipo,” alisema Bi. Zaipuna.

Pia, Bi. Zaipuna alieleza kuwa NMB imejikita katika kuchangia miradi ya nishati safi ya kupikia, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 100 zimetengwa kusaidia biashara na miradi inayosambaza nishati safi kwa Watanzania.

Uzinduzi wa matawi ya NMB Chanika na Kinyerezi unaiwezesha benki hiyo kufikisha jumla ya matawi 241 nchini kote, ikizidi kuimarisha huduma zake na kuleta maendeleo kwa jamii.
















 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MWABUKUSI ATOA NENO SIMBA KUSUSIA DERBY DHIDI YA YANGA

HOSPITALI YA MUHIMBILI YAANZISHA HUDUMA YA KISASA YA KUZIBA MAPENGO

MWANAMKE ALIYEVUNJA REKODI KWA KUZAA WATOTO 69

BODI YA LIGI YAKIRI MAKOSA, WAIOMBA YANGA WAYAMALIZE

BODI YA LIGI SASA WAOMBA HEKIMA NA BUSARA ITUMIKE DERBY YA YANGA, SIMBA