Na Mwandishi Wetu, WMTH-Singida
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,
Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewahimiza wananchi wa Ikungi kutumia mtandao kwa manufaa na kwa njia salama.
Naibu Waziri Mahundi alitoa rai hiyo tarehe 27 Machi 2025, alipofanya ziara ya kukagua hali ya mawasiliano katika Jimbo la Singida Mashariki.
“Tuache kutumia vifaa vyetu vya simu kwa uhalifu mtandaoni. Kama wizara, tunaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha matumizi bora na salama ya mawasiliano,” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuboresha mawasiliano vijijini kwa kusema: “Tunataka kila kata ipate mnara wa mawasiliano au kuboresha minara iliyopo ili kuhakikisha mawasiliano yanapatikana kwa urahisi kwa wananchi wote.”
Naibu Waziri Mahundi aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la kidijitali. “Mheshimiwa Rais Samia anataka Tanzania ya Kidijitali, hivyo ni lazima huku Ikungi tuende na wakati. Tukitumia mtandao vizuri, tunaweza kujikomboa kiuchumi,” alisisitiza.
Naye Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe. Miraji Mtaturu, aliipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuboresha mawasiliano vijijini. Alisema kuwa tayari baadhi ya vijiji vimenufaika na mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi alieleza kuwa kuboreshwa kwa huduma za mawasiliano kunasaidia kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo kilimo, biashara, na huduma za kifedha.
Comments