- Asema muwekezaji amefanya kazi kubwa lazima Serikali imuunge mkono.
- Awagiza watendaji wa Halmashauri kusimamia ukamilishaji wa miradi.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amemuagiza Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na watendaji wa Wizara hiyo kukutana na kufanya mapitio ya vigezo ili kukipandisha hadhi kituo cha Afya cha Mama Ngoma kilichopo kata ya Kwakoa Wilaya ya Mwanga Mkoani kilimanjaro kuwa hospitali.
Amesema mwekezaji huyo amefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shilingi Bilioni tano kwa kujenga majengo yenye hadhi na kuweka vifaa vya kisasa hivyo ni lazima Serikali imuunge mkono kwa kukipandisha kituo hicho.
"Maliza hatua iliyobaki ipewe hadhi ya hospitali kama kuna eneo mnadhani linatakiwa kufanyiwa marekebisho mshirikiane nae, kazi anayofanya huyu ni kubwa ya kuiunga mkono Serikali ya kuwahudumia Watanzania tunamuachaje?". Alihoji
Ametoa maelekezo hayo (jana Jumanne Machi 25, 2023) alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuzindua Kituo Cha Afya cha Mama Ngoma kilichopo kata ya Kwakoa Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Majaliwa amemshukuru Muwekezaji wa kituo hicho Profesa Ngoma na kumuahidi kuwa Serikali itaendelea kumuunga mkono.
"Umeniambia unataka uanzishe chuo cha uuguzi hapa, endelea na taratibu, ongeza ubunifu na ongeza huduma, Serikali tutakuunga mkono".
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amekagua jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ambalo hadi kukamilika kwake litatumia shilingi bilioni 3.7 ambapo amewaagiza viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati.
Kadhalika, amewataka madiwani na viongozi wa Halmashauri na Wilaya zote nchini kuhakikisha wanasimamia ukamilishaji wa miradi yote ambayo iko katika hatua ya ukamilishaji. “Msisitizo wangu miradi yote ambayo bado haijakamilika ikamilike kabla ya mwezi wa nane”
Mheshimwa Majaliwa amehitimisha ziara yake ya siku moja kwa kuzungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Usangi Wilayani Mwanga ambapo amewasihi wananchi kuendelea kuwa na imani na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Rais wetu ana nia ya dhati ya kuwatumikia watanzania na ana mpango kazi mzuri wa kukamilisha miradi ya maendeleo sambamba na kusogeza huduma karibu na wananchi."
Comments