Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameziagiza
Wizara za Uchukuzi na Viwanda na Biashara kuanza kutoa huduma zote za kibandari
katika Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha shughuli za usafirishaji kuanzia tarehe 4
Agosti, 2025.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala
(Kwala International Logistics Centre) mkoani Pwani, ambapo amesema ni hatua ya kihistoria
itakayopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori katika Jiji la Dar
es Salaam, na kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji wa viwanda na ajira kwa
Watanzania.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa uzinduzi wa kituo hicho utarahisisha shughuli za
uchukuzi na kupanua wigo wa biashara kwa Watanzania na nchi jirani.
Ameongeza kuwa kituo hicho kinalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni maandalizi ya ushiriki kamili wa nchi katika
Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
“Bandari Kavu ya Kwala itarahisisha usafirishaji wa mizigo ya nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda na Malawi na kuongeza mvuto wa
Bandari ya Dar es Salaam katika ushindani wa kikanda,” alibainisha Rais Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amezindua rasmi safari za mizigo za treni ya umeme
ya SGR, ambapo amesema kuwa hatua hiyo muhimu itakayobadili mfumo wa uchukuzi
nchini ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza
uchakavu wa barabara na kulinda mazingira.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imewekeza Shilingi Bilioni 330.2 kwa ajili ya ununuzi
wa mabehewa 1,430 ya mizigo ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa
wafanyabiashara na ametoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa ya uwepo wa reli hiyo
kuwekeza katika usafirishaji wa mizigo na abiria, ikiwemo kununua vichwa na mabehewa
yao wenyewe.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia aliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya
Kwala (Kwala Industrial Park) inayotarajia kuwa na viwanda 200 itakapokamilika, ambapo
viwanda saba tayari vimekwishaanza kazi na vitano vipo katika hatua ya ujenzi.
Akizungumzia fursa za ajira, Rais Dkt. Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Pwani na
Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa hizo, ikiwemo kuanzisha biashara
ndogondogo na huduma zinazozalishwa na mradi huu, akitaja kuwa ajira 50,000 za moja
kwa moja na 150,000 zisizo za moja kwa moja zitazalishwa kutokana na viwanda 200
vitakavyojengwa katika Kongani hiyo ya Viwanda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipunga bendera (flag off) kuashiria uzinduzi rasmi wa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri wa Treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwenye hafla fupi iliyofanyika katika eneo la Marshalling Yard, Kwala Mkoani Pwani tarehe 31 Julai, 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri wa Treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma katika eneo la Kwala Mkoani Pwani tarehe 31 Julai, 2025.
Comments