Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kutoka Shilingi 275,060 hadi Shilingi 358,322, ikiwa ni ongezeko la asilimia 33.4, hii ni kwa mujibu wa tovuti ya Mwananchi.
Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa ongezeko hilo kwa sekta binafsi ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Ridhiwani, mapitio ya kima cha chini cha mshahara hufanyika kila baada ya miaka mitatu, ambapo tangazo la mwisho lilitolewa mwaka 2022.
Ameeleza kuwa Serikali inataka waajiri wote wa sekta binafsi kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza kima hicho kipya cha mshahara kwa mujibu wa sheria.
Ameonya kuwa Ofisi yake haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza agizo hilo kwa makusudi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake.
“Aidha ofisi yangu itaendelea kufatilia kwa karibu utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi pamoja na kufanya tathimini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu," amesema.
Imeelezwa kuwa kima hicho kipya kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026, ikiwa ni hatua ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuleta uwiano na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma lililotangazwa awali.
Rais Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu mkoani Singida, alitangaza kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 kutoka Shilingi 370,000 hadi Shilingi 500,000 kama sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha maisha ya wafanyakazi nchini.
Comments