SINA budi kuvipongeza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa yenye uweledi kwa kudhibiti kwa kiwango cha Juu hali ya usalama wa Nchi Desemba 9, 2025 na kuendelea.
Siku hiyo kulikuwa na tishio la uwepo wa maandamano haramu yaliyotangazwa na vibaraka wa mabeberu wasioitakia mema Nchi yetu nzuri Tanzania inayowindwa kila kukicha na mabeberu hao kwa lengo la kupora rasilimali lukuki tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu yakiwemo madini ya thamani kubwa.
Mashujaa hao waliofanya kazi hiyo kwa ushirikiano mkubwa ni; Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, bila kuwasahau wananchi waliotii sheria kwa kukataa kabisa kushiriki maandamano hayo haramu.
Pia pongezi za pekee ziliendee Jeshi la Polisi kupitia Msemaji Mkuu wake, David Misime,kwa kitendo cha kutoa mara kwa mara taarifa kwa Wananchi kuhusu hali ya usalama wa Nchi ilivyokuwa inaendelea, hivyo kuwaondolea hofu wananchi.
Walienda mbali zaidi kwa kuwaeleza wananchi kuhusu picha za mjongeo feki/ zilizopitwa na wakati zilizokuwa zinasambazwa na vibaraka hao wasiioitakia amani Tanzania.
Kitendo cha picha hizo za uongo kusambazwa kwenye mitandao kwa lengo la kuzua taharuki kiliniudhi na kupelekea mimi nitoke nyumbani kwenda mitaani kupata uhalisia wa kinachoendelea ili nami kupitia taaluma yangu pendwa ya uandishi wa habari niwafahamishe wananchi taarifa sahihi.
Ilikuwa majira ya saa 9 alasiri, nikachukua vitambulisho vyangu muhimu na simu zangu na kuacha kamera na vifaa vingine vya kazi,kwani niliamini simu zitatosha kukamilisha kazi niliyokuwa naenda kufanya.
Nilipofungua geti nikakutana na mpangaji mwenzangu ambaye ghafla akanieleza kuwa amesikia kuwa Chuo Kikuu Cha Dodoma yaani UDOM na Area C Dodoma wameandamana.
Nikambishia na kumhakikishia kuwa hakuna maandamano ni uzushi mtupu, kwani muda si mrefu nimetoka kuipublish kwenye mitandao yangu taarifa ya Polisi ikieleza kuwa hadi mchana wa siku hiyo ya Desemba 9, hali ya usalama wa Nchi ni shwari.
Nikamuaga kuwa naenda mjini, alishtuka huku akiniambia huogopi kukamatwa?!! Nikamjibu kuwa siogopi kwa vile nami naenda kikazi, sina ajenda nyingine mbaya, zaidi ya kwenda kutimiza wajibu wangu wa kupata taarifa sahihi ya hali ya utulivu iliyokuwa inaendelea katika Jiji la Dodoma ambayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama.
Aliniaga kwa wasiwasi, huku mimi nikielekea barabarani kutafuta usafiri wa kwenda Mjini. Daladala zilikuwa zinapita moja moja na baada ya kusubiri kwa muda bila kutokea nikaamua kukodi boda kutoka eneo la Mailimbili ambapo njiani nikamuuliza huogopi kwenda Mjini? Akanijibu kuwa haogopi kwani muda si mrefu alitokea huko na hakuna matatizo.
Nikiwa njiani nikawa nachukua picha ya video kwa kutumia simu kuonesha hali ya utulivu inavyoendelea katika maeneo ya Wajenzi, Area C, Area A, Chinangali Park, Machinga Complex, Uwanja wa Ndege, Chako ni Chako, Mataa ya kuongozea magari na hatimaye nikaingia mjini.
GHAFLA NIKAZINGIRWA NA ZAIDI YA ASKARI 10
Nilipofika Nyerere Square huku nikiendekea kupiga picha kuonesha jinsi Jiji lilivyotulia, nikasikia sauti za askari Jeshi wakinikataza kupiga picha, nikatii na kuweka simu mfukoni na kushuka kwenye boda nikamruhusu aondoke.
Nikiangalia ndani ya viwanja vya Nyerere Square, hapakuwepo raia wa kawaida kama ilivyozoeleka,bali walionekana askari wa majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama wakiendelea kulinda doria.
Katika barabara zinazozunguka viwanja hivyo walionekana baadhi ya raia wachache wakiendelea na mihangaiko yao bila kubughudhiwa. Pia zilikuwepo bodaboda, bajaji na daladala chache zikisubiri abiria.
Wakati naangaza huku na kule nikisubiri daladala za kwenda Mailimbili ninakoishi, mara ghafla wakaja askari mchanganyiko zaidi ya 10 wengi wao wakiwa wanajeshi na kunisimamisha na kuanza kunihoji huku wakinielekeza niende nao ndani ya viwanja vya Nyerere Square.
Kwa vile nilijiona sina kosa, sikuwa na hofu yoyote bali nilijawa na furaha moyoni kwa kuona vyombo vyetu vya Ulinzi na usalama viko makini na kazi yao.
Kiongozi wao aliniuliza imekuwaje sisi tumekuita wakati unapiga picha umekaidi? Nikawajibu bila woga kwamba sikuwaelewa nilidhani walikuwa wananikataza kuendelea kupiga picha.
Nikawaambia ili wasiendelee kuniuliza maswali mengi, nijitambulishe kwanza.Wakakubali. Nikawaeleza kuwa ni Mwandishi wa habari huku nikiwaonesha vitambulisho kikiwemo cha NIDA.
Enhe,kwa hiyo hizo picha ulikuwa unapiga kwa malengo gani? Nikawajibu kuwa lengo la picha hizo ni kuufahamisha umma uhalisia wa utulivu wa Jiji la Dodoma tofauti na picha za uongo zinazosambazwa na wasioitakia mema Nchi yetu.
Nikawapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imepelekea uwepo wa amani na utulivu, na kwambqkazi hiyo hatuwezi kuwaachia wao, bali hata wanahabari inatupasa kutimiza wajibu wetu kwa kuwapelekea wananchi taarifa sahihi zenye maslahi kwa Taifa.
Baada ya kunihoji mambo mengine ya msingi, wakachukua simu zangu na kuangalia picha mjongeo nilizopiga, wakajiridhisha kuwa hazina madhara. Ndipo wakaniruhusu kuondoka.
Ndimi, Richard Mwaikenda
0754264203
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika

Comments