SERIKALI imeongeza kwa kiasi kikubwa mikopo ya elimu ya juu, ambapo ndani ya mwaka huu wa fedha 2025/2026, wanafunzi 276,032 wamenufaika na mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 899.
Ongezeko hilo limetangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 31,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba Makao Makuu ya Nchi Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za uongozi wake wa Awamu ya Sita.
Aidha, kupitia Samia Scholarship, Serikali imetoa ufadhili kwa wanufaika 3,137 ndani na nje ya nchi katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati, tiba na TEHAMA, ikiwa ni pamoja na sayansi ya data na akili unde (AI).
"Serikali ya Awamu ya Sita pia imekamilisha ujenzi wa shule 26 maalum za sayansi kwa wasichana na shule 5 za vipaji kwa wavulana, huku nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi."Amesema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa kampasi mpya za vyuo vikuu katika mikoa 15, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa majengo na uwekaji wa mawe ya msingi katika mikoa ya Kagera, Lindi na Zanzibar.
"Mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 yanaonesha wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya Taifa."
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda akifafanua jambo katika mkutano huo.Baadhi ya waandishi wa habari na viongozi wa wizara hiyo.



Comments