CCM YAMEGEWA SIRI YA USHINDI WA KIKWETE

Na Richard Mwaikenda

WAGOMBEA walioshindwa katika kura za maoni za kuwania ubunge na udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuiga uvumilivu wa Mwenyekiti wao wa Taifa, Jakaya Kikwete  aliyefanya hivyo kwa miaka 10 baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais mwaka 1995.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana UVCCM Taifa, Ridhiwani Kikwete.

Alitoa kauli hiyo katika Jimbo la Kigamboni,
Dar es Salaam wakati wa mkutano wa ndani wa kampeni za kupanga mikakati ya ushindi wa kishindo wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao.

"Kushindwa uchaguzi kunauma sana, lakini nawaomba muwe wavumilivu kama alivyofanya kwa miaka10 Mwenyekiti wetu, Rais Jakaya Kikwete ambaye licha ya kuongoza katika kura za maoni za kuwania urais mwaka 1995, jina lake lilienguliwa kwa kufuata utaratibu wa chama,"alisema Ridhiwani.

Alisema ilipotokea hivyo, watu wengi waliokuwa wanamuunga mkono waliudhika na baadhi yao kuamua kuchana fulana na kutishia kuchoma bendera ya chama lakini Kikwete aliwatuliza na hakuthubutu kukihama chama hadi amekuwa Rais.

"Uvumilivu wake huo ndiyo uliopelekea chama mwaka 2005 kuona  muda muafaka ulifika kwa Kikwete kupatiwa fursa hiyo ya kuwania urais na hatimaye kushinda katika Uchaguzi Mkuu na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, " Ridhiwani alisema.

Pia aliwatolea mfano mwingine wa uvumilivu alioufanya Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Nape Nnauye ambaye mara kwa mara amekuwa akishindwa katika harakati zake za kuomba uongozi ikiwemo nafasi ya ya kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo kupitia CCM.

Alisema baada ya kipindi kirefu cha Nape kuvumilia,  ameteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi kazi ambayo ameshaianza.

Aliwaasa  wote walioshindwa kuachana na makundi bali warudishe mioyo yao kwa kujenga umoja na walioshinda kwa lengo la kukipatia chama ushindi wa kishindo.

"Jamani huu si muda wa kulumbana na kuoneshana ubabe baina ya makundi ya wagombea bali kinachotakiwa sasa ni kuunganisha nguvu na kuhakikisha chama kinashika dola,"alimalizia kusema Ridhiwani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

CHAMA KIPYA CHA WALIMU WAMUOMBA RAIS SAMIA AINGILE KATI MAKATO YA WANACHAMA WAO

NILIYOYABAINI KATIKA TRENI YA SGR DAR ,MORO HADI DODOMA … KADOGOSA REKEBISHENI MAMBO HAYA MTANIKUMBUKA

IBENGE: YANGA SC WATAFUZU HATUA YA ROBO FAINALI.