JK ATANGAZA KUGAWA VIANDARUA BURE KWA WATU WOTE

--------------------------------------------------------------------------------
UGAWAJI wa vyandarau vya bure kwa Watanzania wote katika jitihada za Serikali kupambana na kutokomeza ugonjwa hatari wa malaria umeanza, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza.

Mpango huo ujulikanao kama “Chandarau Kila Kilipo Kitanda” ni moja ya hatua kadhaa zinazochukuliwa na Serikali kujaribu kutokomeza ugonjwa wa malaria unaoua Watanzania wengi zaidi kuliko ugonjwa mwingine wowote.

Rais Kikwete ambaye ni Mgombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ametangaza habari hizo  njema katika mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu iliyofanyika leo, Alhamisi, Oktoba 21, 2010, katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mtwara ambako amehutubia mikutano mikubwa ya wananchi.

Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Newala, Rais Kikwete amesema kuwa ugawaji wa vyandarau hivyo kiasi cha milioni 14 umeanza katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo ni baadhi ya mikoa inayosumbuliwa zaidi na ugonjwa wa malaria.

Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye mkutano huo kuwa utoaji wa vyandau hivyo ambao umeanza majuzi unatakiwa uwe umekamilika kwa nchi nzima ifikapo mwishoni mwa Desemba.

“Baada ya hapo Serikali itafanya tathmini kuona kama yatakuwepo mahitaji zaidi ya vyandarau hivyo ama kama vitakuwa vimetosha,” Rais amewaambia wananchi kwenye mkutano huo.

Rais  Kikwete ambaye pia amerudia kutangaza habari hizo njema katika mikutano mingine ya kampeni katika maeneo ya Chiungutwa katika jimbo la uchaguzi la Lulindi, mjini Tandahimba na Nanguruwe katika jimbo la Mtwara Vijijini amesema kuwa yamefanyika marekebisho kidogo katika jinsi ya kugawa vyandarua hivyo.

Awali, Serikali ilipanga kutoa vyandarua viwili kwa kila kaya, lakini katika Mkoa wa Mtwara, vyandau vimegawiwa kulingana na idadi ya vitanda kwa kila kaya.

Utoaji wa vyandarau hivyo ni sehemu za hatua ambazo mpaka sasa zimechukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa inatokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2015 ambako Rais Kikwete amepanga kuwa uwe mwaka wa Tanzania kuitangazia dunia kuwa imetokomeza ugonjwa wa malaria.

Baadhi ya hatua ambazo mpaka sasa zimechukuliwa na Serikali katika kupambana na ugonjwa huo hatari ni kutoa vyandarau bure kwa watoto wote wenye umri wa miaka mitano, na kutoa vyandarau vya bei ya chini sana chini ya mpango wa Hati Punguzo kwa akinamama wote waja wazito

Serikali pia imeanza mpango kabambe wa kupuliza dawa za kuua mbu katika nyumba zote nchini kwa kuanzia katika Mkoa wa Kagera, mkoa ambao unaongoza nchini kwa kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba inakusudia kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa ya kuharibu mazalio ya mbu katika kuhakikisha kuwa mbu wanauawa kwenye sehemu zao za kuzalia.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

KANUNI 10 ZA MAHUSIANO YENYE FURAHA

HAKI 13 ZA MWANAMKE LAZIMA MWANAUME AZIHESHIMU:

MAMBO SABA AMBAYO WANAUME WENGI HAWAYAPENDI:

NI HESHIMA KUBWA SANA KUIFUNDISHA YANGA - KOCHA MPYA WA YANGA

RAIS DKT.MWINYI: ZANZIBAR KUWA KITUO CHA BIASHARA CHA KIMATAIFA

”RAIS SAMIA AUMIZWA MAUAJI YA KIBIKI”

KOCHA SEAD RAMOVIC AMRITHI GAMONDI YANGA.

UOKOAJI KARIAKOO NI USHUHUDA WA MOYO WA UTANZANIA: NCHIMBI

ACHENI KUWA CHANZO CHA CHOKOCHOKO NA VURUGU - ASKOFU CHANDE