Kitendo cha SIMBA SC kutinga hatua ya Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimeleta majanga katika Ligi Kuu Bara baada ya mabosi wa Bodi ya Ligi kujifungia ili kuipangua ratiba tena.
.
Simba itavaana na RS Berkane ya Morocco, lakini ikiwa na mechi nane mkononi, zikiwamo tano za viporo vya Ligi Kuu zilizopangwa kupigwa ndani ya Mei pamoja na kiporo dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8 mwaka huu.
.
Kuwepo kwa mechi mbili za fainali dhidi ya RS Berkane kati ya Mei 17 na 25 umetibua mechi hizo za viporo za Simba sambamba na ile ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars ya Mei 18, jambo hilo limewalazimisha watu wa Bodi ya Ligi kuanza mkakati wa kupangua ratiba.
.
Simba itaanza kampeni za kusaka taji hilo kubwa Afrika kwa kucheza fainali ya kwanza ugenini Mei 17 ikiwa Morocco, kisha kurudi jijini Dar es Salaam kwa mechi ya marudiano itakayopigwa Mei 25, ambayo ilikuwa ndio tarehe ya mwisho mwa msimu.
.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu, inaonyesha Simba inaanza Mei 2 kwa kucheza na Mashujaa nyumbani kabla ya kuwafuata maafande wa JKT Tanzania Mei 5, kisha Pamba Jiji Mei 8, huku ikiifuata pia KMC Mei II kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora. Baada ya hapo, Simba ingekuwa na mechi na Singida Black Stars Mei 14, kisha kusafiri Mbeya kuifuata KenGold iliyoshuka daraja Mei 21 na kuikaribisha Kagera Sugar Mei 25, kabla ya kupambana na Yanga ambayo tarehe mpya bado haijapagwa pia.
.
Kitendo cha ratiba hiyo kubana, kikaifanya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kupitia kwa Ofisa Habari, Karim Boimanda kuweka wazi watu wa idara watakaa chini kwa ajili ya kupanga vizuri ratiba, ili kutoa pia nafasi ya kujiandaa vyema kwa wawakilishi hao pekee wa nchi Kimataifa.

Comments