BALOZI NCHIMBI: FIDIA MIFUGO ILIYOTAIFISHWA IHITIMISHWE

 

 _Asema ni muhimu kutekeleza maamuzi ya mahakama_

_Kampeni ya ‘Tutunzane’ itumike pia kwenye siasa_

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametoa maelekezo kwa Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kuratibu mazungumzo ya kuwalipa fidia wafugaji ambao mifugo yao ilitaifishwa lakini walishinda kesi mahakamani, ili suala hilo limalizike.

Balozi Nchimbi amesema kuwa madai ya wafugaji hao, ambao walishinda kesi mahakamani baada ya mifugo yao kutaifishwa kwa tuhuma za kuingiza mifugo maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria, yamechukua muda mrefu na yanapaswa kuhitimishwa kwa kutekeleza maamuzi ya mahakama.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la Wafugaji, mkoani Simiyu, katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi, Jumapili, tarehe 15 Juni 2024, ambapo pia alisisitiza kuwa dhamira ya CCM ya kuboresha sekta ya mifugo na kubadilisha maisha ya wafugaji haitayumba wala kutetereka, kwani chama kinatambua mchango wao katika uchumi wa taifa.

“Kwenye risala yenu mmezungumzia masuala saba. Asante Waziri kwa kulichukua suala la ardhi ya kujenga ofisi. Kuna hili la madai ya mifugo kutaifishwa. Tumefuatilia, na kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu masuala ya bei. Hivyo naomba kutoa maelekezo kwa Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kuratibu mazungumzo hayo ili suala hilo limalizike.

“Ni muhimu suala hili lijadiliwe na likamilike. Maamuzi ya mahakama yatekelezwe. Mahakama ndiyo chombo cha mwisho cha kutafsiri sheria na kutoa haki nchini. Ni lazima tuoneshe mfano wa utekelezaji wa maamuzi ya mahakama,” alisema Balozi Nchimbi.

Aidha, Balozi Nchimbi alisema kuwa kampeni ya ‘Tutunzane’, ambayo ni moja ya mikakati iliyosaidia wakulima na wafugaji kutambua umuhimu wa kutegemeana, na iliyoanzishwa na Serikali wilayani Mvomero, inafaa kutumika nchi nzima, hata katika siasa, ili Tanzania iendelee kuwa nchi yenye amani, utulivu, upendo na mshikamano.

“Nawapongeza Mvomero kwa wazo la ‘Tutunzane’. Tukitambua kuwa sote tunategemeana, taifa letu litaendelea kusonga mbele kwa kasi ya maendeleo. Hata kwenye vyama vya siasa tunapaswa kuiga hili; sisi CCM tunaweza kuwatunza vyama vya upinzani kama ACT, CHADEMA, CUF na vyama vingine. Hili ni jambo jema tunaweza kuiga sisi wanasiasa,” alisema Balozi Nchimbi.

Aidha, Balozi Nchimbi alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa jinsi inavyoendelea kuwatumikia wafugaji kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na ongezeko la bajeti ya wizara hiyo. Alisisitiza pia umuhimu wa wafugaji kuzingatia sheria katika shughuli zao ili ziendelee kuwa na tija kwa jamii, taifa na nchi kwa ujumla.

Katibu Mkuu huyo wa CCM aliwakumbusha Watanzania kujiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa hamasa kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, ili wananchi watekeleze wajibu na haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

UKWELI KUHUSU TENDO LA NDOA NA FAIDA ZAKE

HUYU NDIYE WANU HAFIDH, CHAMPIONI WA ELIMU

MAWAZIRI WALIOACHWA HAWA HAPA

๐Œ๐‰๐”๐„ ๐Š๐€๐‚๐‡๐„๐‘๐Ž ๐Œ๐™๐„๐๐€

HISTORIA YA MAREHEMU MC PILIPILI

VITU 10 WANAUME WANAVYOPENDA ZAIDI TOKA KWA MWANAMKE — SIYO SURA, SIYO MWILI ❤️

USIKUBALI KUWA LOFA KWA MWANAMKE...

NAPE AWAPA UKWELI VIJANA