Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema kwa kushirikiana na sekta binafsi Januari mwaka 2026 wanatarajia kuanza ujenzi wa reli ndani ya Jiji la Dar es Salaam itakayounganisha maeneo yote ya kimkakati kiuchumi na kulifanya kuwa Metro city.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Masanja ameyasema hayo leo Jijini Arusha, wakati akiwasilisha mada ya mipango ya shirika katika uchumi jumuishi kwenye Mkutano wa 18 wa pamoja wa mapitio ya sekta ya usafirishaji unaoendelea Jijini Arusha kwa kauli mbiu ya mifumo jumuishi ya usafirishaji kama msingi wa mageuzi ya kiuchumi kuelekea DIRA 2050.
Amesema kuanzia mwakani ujenzi utaanza kutoka Mwenge, Mlimani City, Soko la Afrika Mashariki hadi Morocco na kisha Kariakoo, ikiwa ni maeneo yenye watu wengi na muhimu kiuchumi.
“Kwasasa Dar es Salaam inakabiliwa na changamoto ya foleni, ingawa wanasema Metro City zote hazikosi foleni, nasi katika kukabili foleni Dar tunajenga reli kwa ajili ya kuongeza urahisi wa usafiri. Itajengwa kando mwa mwendokasi,” amebainisha.

Comments