SERIKALI IMEENDELEA KUCHUKUA HATUA ZA MAKUSUDI ZA KUIMARISHA UHURU WA MAHAKAMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama, na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwa Kata zote nchini zisizo na Mahakama za Mwanzo.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwamba, uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki. Amesema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Makamu wa Rais amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Ameongeza kwamba Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa Kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, Kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, Kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi, Kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na Kudumisha amani na mshikamano wa Kitaifa, ambao ni msingi wa maendeleo endelevu. @nchimbie @ofisi_ya_makamu_wa_rais








Comments