Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema ameondoka nchini humo kwa muda baada ya kujificha kwa takribani miezi miwili.
Katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Bobi Wine alisema anasafiri kwenda nje ya nchi kwa kile alichokiita mikutano muhimu, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu safari hiyo.
Mwanasiasa huyo, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alionekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa kupitia video ya dakika tano iliyochapishwa kwenye mtandao wa X.
Bobi Wine alisema alilazimika kukimbia nyumbani kwake mjini Kampala baada ya vikosi vya usalama kuvamia makazi yake kufuatia uchaguzi wa Januari, ambao anadai ulijaa udanganyifu na upendeleo kwa rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni.
Mwanamuziki huyo wa zamani aliyegeuka kuwa mwanasiasa alisema alifanikiwa kukwepa kukamatwa na sasa ameondoka nchini, lakini ameahidi kurejea kuendelea na mapambano yake ya kisiasa.
Hivi karibuni, mkuu wa jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mtoto wa Rais Museveni alisema kuwa wanamtafuta Bobi Wine, bila kufafanua iwapo kuna mashtaka yoyote rasmi dhidi yake.
Pia unaweza kusoma:

Comments