Mwandishi wetu, Morogoro
MKUU
wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka Watanzania kuendelea
kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha mwezi
mtukufu wa Ramadhani na hata baada ya kumalizika kwa mwezi huo.
RC
Malima ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye futari iliyoandaliwa
na Benki ya CRDB kwa ajili ya wateja wake pamoja na wadau mbalimbali wa
benki hiyo mkoani Morogoro.
Amesema
kipindi cha Ramadhani ni muda muhimu kwa waumini wa Kiislamu
kujitathmini, kufanya ibada na kuimarisha mahusiano mema, huku
akisisitiza kuwa maombi yana mchango mkubwa katika kulinda amani na
maendeleo ya taifa.
“Niwaombe
Watanzania wote kutumia kipindi hiki cha Ramadhani kumuomba Mwenyezi
Mungu alinde amani ya nchi yetu na atupe moyo wa upendo na mshikamano
ili tuendelee kujenga taifa lenye maendeleo,” alisema Malima.
Aidha,
alimshukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa futari hiyo ambayo imewaleta
pamoja viongozi, wateja na wadau mbalimbali katika kuimarisha mahusiano
na mshikamano ndani ya jamii.
Kwa
upande wake, Meneja wa Kanda ya Kati Benki ya CRDB Bi Chabu Mishwaro
amesema lengo la kuandaa futari hiyo pamoja na dua maalum ni kushiriki
ibada na kuungana na wateja wao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Amesema
benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kukutana na wateja wake katika
kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuimarisha na
kuendeleza ushirikiano wa kibiashara pamoja na kushirikiana katika
matendo ya kijamii yenye kuleta baraka kwa jamii.
“Futari
hii ni sehemu ya kuonesha kuthamini wateja wetu ambao wamekuwa nguzo
muhimu ya mafanikio ya benki yetu. Tunathamini sana mahusiano haya na
tunaamini kuungana katika ibada na dua kunaimarisha mshikamano wetu,”
alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa benki hiyo Mussa Kitambi amesema
imekuwa ni utamaduni wa CRDB Bank kuandaa futari kwa ajili ya wateja
wake kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani.
Amesema
mwezi mtukufu wa Ramadhani ni chuo cha malezi ya kiroho na nidhamu kwa
waumini wa Kiislamu, huku swaumu ikiwa ni ibada inayowafanya watu wengi
kuelekeza mioyo yao katika kumtii Mwenyezi Mungu, kufanya wema na
kusaidia wenye uhitaji.
Aliongeza
kuwa benki hiyo imekuwa ikiendelea kutoa huduma mbalimbali
zinazozingatia mahitaji ya wateja Waislamu, ikiwemo programu maalum za
huduma za kifedha zisizo na riba ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao
ya kiibada na kimaendeleo kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu.
“Tunatoa
huduma za uwezeshaji wa kifedha zisizo na riba kwa wateja wetu ili
kuwasaidia kutekeleza shughuli zao za kiuchumi bila kwenda kinyume na
misingi ya imani yao. Tunawaomba wateja wetu waendelee kuiamini na
kushirikiana na benki yetu,” alisema.
Futari
hiyo pia iliambatana na utoaji wa zawadi na misaada mbalimbali kwa
watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya
juhudi za benki hiyo kurejesha kwa jamii na kuonesha mshikamano katika
mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.








Comments